SOMO # 13: FURAHA ISIYO NA UKOMO
Heri ya mwaka mpya Wapendwa!
Wapendwa siku zote katika
Maisha haya tunayoishi hapa duniani wakati mwingine huwa tunapitia changamoto
nyingi sana mpaka zinapelekea kukosa furaha kwa kipindi furani, baada ya
kusahau furaha hurudi tena. Lakini siku ya leo Mungu anatuambia katika kitabu cha
1 Wathesalonike 5:16 kwamba;- Furahini siku zote.
Neno hilo ‘Furahini siku zote’
lina maana kubwa sana katika Maisha yetu endapo kama tutalichukulia kwa uzito
mkubwa sana. Mungu kusema hivyo sio kwamba hajui kama huwa wakati mwingine
tunapata changamoto ambazo zinatuondolea furaha. Lakini Yeye anatamani
tuzichukulie hizo changamoto kama ni sehemu ya Maisha kwani huwa zinamwisho
kwahiyo zisituondolee furaha ndani ya mioyo yetu.
Mpendwa tambua kwamba
Unapokuwa na Yesu kisawasawa ndani yako na ukapata changamoto inatakiwa
usiiangalie hiyo changamoto maana itakuondolea furaha bali mwangalie Yesu ,yeye
ndio ataiangalia hiyo changamoto na kuindoa huku wewe ukiwa unaendekea kuwa na
furaha. Wakati mwingine inaweza ikawa ni
vigumu lakini inaweza ikawa rahisi kama Roho Mtakatifu yupo ndani yako. Roho
Mtakatifu ndio huwa anatoa nguvu ya ziada juu ya jambo fulani mpaka kupelekea
watu wanaokutazama wasielewe nini kinaendelea kwako.
MUHIMU: Furaha
isiyo na kikomo kuwa inaambatana na Yesu kuwa ndani yako maana yeye ndio
atakufanya uchukuliane na mambo mbalimbali ambayo yanaweza kukuondolea furaha,
ndio maana katika kitabu cha Wafilipi 4:4 imeandikwa; Furahini katika
Bwana siku zote tena nasema furahini.
NINI HUTOKEA FURAHA
IKIKOSEKANA?
Furaha inapokosekana ndani ya
mtu, maana yake anaweza kufanya mambo mabaya ambapo ndani ya mambo hayo Mungu
huwa hayupo kabisa , Yesu huwa hakai mahali ambapo hakuna furaha, ndio maana
amesema furahini katika Bwana.
Baadhi ya Mambo yafuatayo
yanaweza kutokea mtu akakosa furaha;
Mtu anaweza asisamehe kabisa
au akasamehe baada ya muda mrefu kupita .
Hii ni kwa sababu hana furaha ndani yake juu ya jambo lililomkwaza.
Huleta uchungu ndani na moyo.
Usipo ruhusu furaha itawale ndani yako maana yake utaendelea kuumia juu ya
jambo fulani ambalo limekutokea, na mwisho wake ukawa mabaya.
Husababisha kulipiza kisasi.
Unapolipiza kisasi maana yake huna furaha ndani yako juu ya huyo mtu , Biblia
inasema kisasi ni juu ya Bwana, kwahiyo unapolipiza kisasi umejipa jukumu
ambalo sio lako ambapo baadaye itakugharimu tu ndio maana katika kitabu cha Warumi
12:19 imeandikwa; Wapenzi,
msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi
ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.
Huondoa
utu na upendo ndani ya mtu. Furaha ikikosekana ndani ya mtu husababisha mtu
huyo wakati mwingine kukosa utu kabisa. Mfano yeye anaona kuuwa ni kawaida tu
au kuiba ni kawaida tu kumbe ni kosa mbele za Bwana.
Husababisha
mtu kujitenga na kuwa ki-vyake vyake tu. Unapojitenga yaani hutaki kuchangamana
na watu wengine maana yake wewe huna furaha ndani ya moyo wako, kwahiyo unaona
bora ujitenge tu kumbe ndio unajisababishia matatizo zaidi kama ilivyoandikwa
katika kitabu cha Mithali 18:1 kwamba; Ajitengaye na wenzake
hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema.
Kuwaza mambo mabaya mabaya.
Mtu akikosa furaha hata kuwaza kwake huwa kunabadilika, yaani anaanza kuwaza
mambo ambayo hata sio mazuri mbele za Bwana, mwisho wa siku anatenda mambo dhambi.
Husababisha kukata tamaa. Mtu
anapokata tamaa maana yake hana huraha ndani yake, mwisho wa siku inampelekea
kufanya mambo mabaya ambapo ni chukizo mbele za Bwana.
Husababisha kujiuwa. Mpendwa
mtu anapokosa furaha na akakosa msaada wowote ,mwisho wa siku inaweza hata
kupelekea akajiuwa kwa kunywa sumu au kujinyonga au kujirusha
sehemu yoyote ya hatari.
Husababisha ndoa kuvunjika au
kulega lega. Wanandoa wakikosa furaha ndani ya ndoa yao inaweza kusababisha
ndoa hiyo ikavunjika au ikawa na migogoro isiyoisha, yaani unawaona watu kwa
nje wanaishi vizuri kumbe ndani ni hatari tupu.
Husababisha mtu kuacha kazi.
Kuna mtu unakuta hana furaha kazini labda kutokana na mazingira ya kazi kuwa
mabaya au imetokea migogoro au ni mvivu wa kufanya kazi. Mtu wa namna hii kwa
sababu hana furaha ndani yake anaweza kuacha kazi, kumbe wakati mwingine
inakuwa sio kwamba ametatua tatizo bali ndio inaongeza matatizo zaidi.
MUHIMU:
Mpendwa kama tulivyoona hapo juu inaonesha kwamba huwa kuna madhara mengi sana
yanaweza kumpata mtu endapo atakosa furaha ndani ya moyo wake, hivyo basi kama
unausoma ujumbe huu na kuna jambo linakutatiza mpaka limekuondolea furaha hebu
tushirikishane ili tuweze kuirudhisha furaha yako kama ilivyokuwa awali. Tambua
kwamba hakuna faida yoyote nje ya furaha.
MPENDWA MUNGU AKUBARIKI SANA KWA KUUSOMA UJUMBE HUU.
NAKUTAKIA MAFANIKIO MEMA YA MWAKA HUU MPYA 2023.
©Msufu-Januari 07,
2023 mawasiliano 0763242555 na 0753255132
Maoni
Chapisha Maoni