SOMO # 18: SOMO: ITAMBUE MAANA HALISI YA KUMPENDA MUNGU
Utangulizi:
Watu wengi sana wamekuwa wakisema wanampenda Mungu lakini ukiangalia uhalisia wa maisha wanayoyaishi na wanachokiongea inakuwa ni tofauti kabisa.
Mtu anasema anampenda/anamheshimu Mungu lakini ukiingalia moyo wake upo mbali naye kutokana na matendo mabaya anayoyatenda kama ilivyoandikwa katika kitabu cha MATHAYO 15:8-9 kwamba;
8. Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali name,
9. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.
Vile vile imeandikwa katika kitabu cha ISAYA 23:13-15 kwamba;
13. Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa;
14. kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa.
15. Ole wao wanaojitahidi kumficha Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?
Mioyo ya watu inawadanganya kwa kusema kwamba wanampenda Mungu kumbe matendo yao ni mabaya kama ilivyoandikwa katika kitabu cha YEREMIA 17:9 kwamba; Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?
Mpendwa Mungu huwa hapendwi kwa maneno tu pasipo kuyatenda aliyotuagiza katika maisha yetu, maana imani bila matendo hiyo imekufa kama ilivyoandikwa katika kitabu cha YAKOBO 2:17 kwamba; Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake, na YAKOBO 2:14 imeandikwa; Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa?
MUHIMU: Kuwa na imani ya kumwamini Yesu Kristo haiishii tu kwenye kutamka kwa kinywa chako, bali inatakiwa kukifanyia kazi kile unachokiamini kupitia Neno la Mungu.
IJUE MAANA HALISI YA KUMPENDA MUNGU
Yafuatayo ni mambo ambayo mtu akiyafanya ndio itaonesha anamwamini Mungu pamoja na kumpenda.
1. Kuchukia uovu/dhambi
Katika kitabu cha MITHALI 8:13a imeandikwa;- Kumcha Bwana ni kuchukia uovu.
Mpendwa maana halisi ya kumpenda Mungu ni kuchukia uovu yaani dhambi za hii dunia. Ikiwa unapenda kutenda dhambi maana yake humpendi Mungu ila unapenda dhambi na dhambi ni adui wa Mungu.
HEBU TAFAKARI HAYA MAMBO HALAFU UJIPIME KAMA KWELI UNAMPENDA MUNGU.
i. Utasemaje unampenda Mungu wakati unapenda kufanya uzinzi na uasherati?yaani ndio umekuwa mtumwa wa hizo dhambi.
1 WAKORINTHO 6:9-10 imeandikwa;- 9. Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, 10. Wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.
YOHANA 8: 34 imeandikwa; Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.
ii. Utasemaje unampenda Mungu wakati unapenda rushwa?
MITHALI 17:23 imeandikwa; Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu.
.
TORATI 23:8 imeandikwa ; Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.
AMOSI 5:12 imeandikwa ; Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao
TORATI 10:17 imeandikwa ; Kwa maana BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye MUNGU wa miungu, na BWANA wa mabwana, MUNGU mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa.
Mithali 29:4 imeandikwa ; Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.'
iii . Utasemaje unampenda Mungu wakati unapenda kubaka/kulawiti watu?
1 WAKORINTHO 6:9-10 imeandikwa;- 9. Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
iv. Utasemaje unampenda Mungu wakati unapenda wizi na ujambazi?
v. Utasemaje unampenda Mungu wakati unapenda uchawi?
vi. Utasemaje unampenda Mungu wakati unapenda kupindisha haki za watu unao wahudumia kwenye hiyo kazi uliyo nayo?
vii. Utasemaje unampenda Mungu wakati muda wote unawaka tamaa mbaya??
viii. Utasemaje unampenda Mungu wakati hata ndugu zako huwapendi?
1 YOHANA 4:20 imeandikwa; Mtu akisema nampenda Mungu na anachukia ndugu yake ni mwongo kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.
ix. Utasemaje unampenda Mungu wakati hata jirani zako huwapendi kila kukicha wewe ni ugomvi tu?
x. Utasemaje unampenda Mungu wakati huna muda wa kutetea wajane ,yatima na Mtu yoyote anayeonewa?
ISAYA 1:17 imendikwa; Jifunzeni kutenda mema ,takeni hukumu na haki wasaidieni walioonewa, mpatieni yatima haki yake,mteteeni mjane.
xi. Utasemaje unampenda Mungu wakati hata huwa huna muda wa kutubu hizo dhambi zako?
UFUNUO 2: 5 imeandikwa; Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
xii. Utasemaje unampenda Mungu wakati hutaki kuomba msamaha wala kusamehe wenzako ?
MATHAYO 6: 14-15 imeandikwa; 14. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi, 15. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
xiii. Utasemaje unampenda Mungu wakati kipaumbele chako ni kwenda disko na kwenye kumbi zingine za starehe kujistaheresha badala ya kukaa na kumtafakari Yesu Kristo?
MATHAYO 6:33 imeandikwa; Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
xiv. Utasemaje unampenda Mungu wakati umekalia kuambatana na marafiki wabaya, mnakaa kupiga stori za uongo na kushawishiana kutenda dhambi?
1 WAKORINTHO 15:33 imeandikwa; Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.
MITHALI 1: 10-11 imeandikwa; 10. Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali, 11. Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu.
2. Kuzishika Amri zake.
YOHANA 14:21 imeandikwa:- Yeye aliye na amri zangu na kuzishika yeye ndiye anipendaye naye atapendwa na Baba yangu nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.
Mpendwa amri za Mungu ni Sheria zake na sheria zake ni Neno lake maana ndani ya Neno la Mungu ndio kuna uzima wa milele na makatazo mbalimbali.
WAEBRANIA 4: 12 imeandikwa; Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. YEREMIA 23:29 imeandikwa; Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?
HEBU JIULIZE?
Je! Umelishika Neno la Mungu? au unabaki kusema tu unampenda Mungu hali ya kwamba huna Neno lolote la Mungu ndani ya moyo wako ambalo ndilo litakusaidia kuenenda katika njia ikupasayo?
YOHANA 15:7 imeandikwa; Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.
MUHIMU: Mpendwa usipoteze muda kwa kusengenya watu, kufanya uzinzi, kuchati na simu mambo yanayokupelekea kutenda dhambi, kuzurura bila mpangilio,n.k bali tenga muda wa kutosha kwa ajili ya Bwana Yesu Kristo ili uweze kulisoma Neno na kulifanyia kazi, kuomba, kufunga n.k. Pia tambua kwamba Neno la Mungu ndilo linaelekeza lipi ni jema la kufanya na lipi ni baya la kutolifanya. Usipolijua Neno kisawasawa itakuwa ni rahisi sana wewe kudanganywa na watu kwa kutekwa na mafundisho potofu.
HATUA ZA KUCHUKUA:
Mpendwa wakati ulipokuwa ukiusoma ujumbe huu yamkini kuna sehemu umeona kwamba matendo yako unayoyatenda yanamchukiza Mungu, na umekuwa ukiishi maisha ya dhambi hivyo hivyo kila siku kwa kumkosea Mungu ( yaani dhambi imekufanya mpaka umekufa ki roho kama ilivyoandikwa katika kitabu cha EZEKIELI 18:20 kwamba; Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake).
Sasa ni wakati wa kumrudia Yesu Kristo kwa kutubu dhambi zako zote na yeye atakusamehe wala hata zikumbuka tena dhambi zako kama ilivyoandikwa katika kitabu cha ISAYA 43:25 kwamba; Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. Pia UFUNUO 2: 5 imeandikwa; Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
Pia kama HUJAOKOKA ni wakati wako sasa wa kumfata Bwana Yesu Kristo kuwa mwokozi wa maisha yako na hata kuacha kwamwe maana Yeye anasema ndiyo njia ya uzima wa kweli ,kila amwaminiye hatapotea abali atakuwa na uzima wa milele kama ilivyoandikwa katika kitabu cha YOHANA 3:16 kwamba; Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Vilevile kitabu cha YOHANA 14:6 imeandikwa; Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. 2 WAKORINTHO 6:2 imeandikwa; Kwa maana asema wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nalikusaidia tazama wakati uliokubalika ndiyo sasa, tazama siku ya wokovu ni sasa.
Hivyo basi okoka mpendwa usimwogope mtu yoyote maana Mbinguni hatuendi kwa sababu ya mali zetu, vyeo vyetu, kazi zetu, akili zetu tunazojivunia, wake zetu, uzuri wetu tunaojivunia, waume zetu, watoto wetu, wazazi wetu n.k bali ni wokovu ndiyo tiketi ya kwenda Mbinguni. Kama upo tayari kuokoka sema ndiyo nipo tayari kwa namba hii 0763242555 nami nitakuombea.
Ubarikiwe sana kwa kuusoma ujumbe huu.
Kwa ushauri piga simu 0763 242 555
Msufu- Septemba 16, 2023
Maoni
Chapisha Maoni