SOMO #9:  MAMBO MUHIMU YA KUYAFANYA KABLA YA KUINGIA MWAKA MPYA 2021.

Mpendwa karibu ujifunze somo hili.

1.      Mshukuru Mungu kwa yote aliyokutendea na ambayo hajayatenda huu mwaka 2020

 

1 Wathesalonike 5:18 imeandikwa;- Shukuruni kwa kila jambo ; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Yesu Kristo.

1 Mambo ya Nyakati 16:34 imeandikwa;- Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema kwa maana fadhili zake ni za milele

Zaburi 75:1 imeandikwa;- Ee Mungu twakushukuru ,twakushukuru kwa kuwa jina lako li karibu ,watu huyasimuliya matendo yako ya ajabu.

Mpendwa, kwahiyo upate au usipate yote hayo ni mapenzi ya Mungu ,hivyo basi Mshukuru kwa vyote.

Baadhi ya Mambo ya kushukuru mbele za Mungu ni kama yafuatayo;-

i.                    Kuna mambo Mungu amefanikisha kukutendea ambayo yalikuwa yapo ndani ya malengo yako ya 2020

ii.                  Kuna mambo amakufanyia ambayo hayakuwepo ndani ya malengo yako ya Huu mwaka 2020.

iii.                Kuna mambo ambayo amekutendea ambayo hayaonekani kwa macho yako Huu mwaka 2020. Mfano Mungu amekuepusha na mambo mabaya mengi sana bila wewe kujua wala kuona kwa macho yako ,kama vile amekupigania na Wachawi na kakuepusha na mitengo ya wachawi bila ya wewe kujua kabisa.

iv.                Mshukuru Mungu kwa ajili ya afya ulilonayo maana hiyo ni Neema ya Mungu tu.

v.                  Mshukuru Mungu kwa ajili ya Wazazi wako,Ndugu zako,Marafiki zako n.k . Mwambie Mungu asante kwa ajili ya Familiya yangu, Wazazi wangu, Walezi wangu,Ndugu zangu wote kwa ujumla n.k . Maana Mungu pia amewatendea mambo makubwa huu mwaka 2020.

vi.                Mshukuru Mungu kwa ajili ya malengo uliyoyaweka mwaka huu lakini bado hayajatimia au yamefikia hatua nzuri kabisa. Mfano Ujenzi wa nyumba labda ulishaanza huu mwaka kujenga lakini bado hujamalizika, au tayari ulianza kukusanya pesa kwa ajili ya kufanya jambo fulani na tayari baadhi ya kiasi cha pesa upo nacho.

vii.              Mshukuru Mungu kwa neema ya Wokovu aliyokupa na umeendelea kusimama na wokovu huo mpaka huu mwaka unapokwenda kuisha leo hii. Hiyo ni neema sema Yesu asante Mshukuru Mungu katika roho na kweli

 

2.      Kusamehe waliokukosea na wewe kuwaomba msamaha uliowakosea.

 

MATHAYO 6:14-15 imeandikwa;- 

14.Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. 

15Bali msipowasamehe watu makosa yao na Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

MARKO 11:25-26 imeandikwa;- 

25.Ninyi kila msimamapo na kusali sameheni mkiwa na neno juu ya mtu ili na Baba yenu aliye mbinguni awasemehe na ninyi makosa yenu. 

26Lakini kama ninyi hamsamehe wala Baba yenu aliye mbinguni hata wasamehe ninyi makosa yenu.

Mpendwa usipende kuingia mwaka mpya huku unakinyongo na mtu au mtu anakinyongo na wewe , Mungu anasema unaposamehe na wewe ndiyo utasamehewa na Yeye , bali usiposamehe na Yeye hata kusamehe, sasa niambie ni nani ambaye hataki kusamehewa na Mungu? Basi wewe utakuwa ni malaika yaani humkosei Mungu, kwahiyo huna haja ya kumwomba msamaha.

Msamaha unaleta afya ya kiakili pia na ya kimwili, vile vile unakuweka wewe kuwa huru muda wote, kwa sababu moyo wako unakuwa hauna malimbikizo ya makosa yoyote ju ya watu waliokukosea.

Mpendwa tunaishi kwenye jamii ya watu wengi hivyo basi kukoseana ni lazima kutokee, hivyo basi msamaha ni endelevu kwa sababu leo atakukosea huyo kesho atakukosea tena mwingine n.k..

Msamaha unaendana na kujishusha, yaani ni lazima mmoja ashuke ili kuweka mambo sawa. Hakikisha unaingia 2021 moyo wako upo safi.

3.      Tubu dhambi zako zote.

Isaya 1:18 imeandikwa;- Haya njooni tusemezane asema Bwana,dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana ,zitakuwa nyeupe kama theluji ,zijapokuwa nyekundu kama bendera zitakuwa kama sufu.

1 Yohana 1: 8-10 imeandikwa;-

8. Tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe ,wala kweli haimo kwetu.

9. Tukiziungama dhambi zetu Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote

10. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi ,twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.

Warumi 3:23 imeandikwa;- Kwa sababu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.

Mpendwa hakikisha unamwomba Mungu akutakase dhambi zako zote ili mwaka mpya uingie ukiwa safi kabisa

 

4.      Fanya tathmini ya mwaka mzima huu unaoisha leo.

i.   Kama ni mfanaya biashara, hebu jaribu kuitathimini biashara yako huu mwaka kama kuna mahali pa kujirekebisha, basi mwaka 2021 ndio uwe  mpya wenye mafanikio ya biashara yako, au kama ulianzisha biashara na ikafa basi jaribu kuangalia ni kitu kipi kilisababisha biashara ife ili mwaka 2021 ukaifufue biashara yako kwa ushindi mkubwa, au ukaanzishe na nyingine kabisa.

ii.  Kama wewe ni mfanyakazi umeajiriwa au umeajiajiri au wewe ndio umeajiri, hebu fanya tathimini uone je huwa unafanya kazi kwa kujituma au mpaka ulazimishwe lakini unapenda mshahara? Je huwa unawahi kazini kulingana na muda wa kazi uliowekwa kwenye taasisi yako?. Je mahusiano yako yapoje na wafanyakazi wenzako? Kama ni mabaya basi jitahidi mwaka 2021 uanze mambo mapya kwa kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzako. Kama wewe ni boss wa ofisi fulani je unawaongoza vipi watu wako wa chini? Unawanyima haki au huwajali kabisa au unajali mambo yako tu? Kama kuna mahali huendi vizuri basi 2021 ujirekebishe katika jina la Yesu Kristo.

iii.  Kama wewe ni mwanandoa , tathimini ndoa yako je unaishi vipi na mwenzi wako ? kama kuna mahali hamuelewani na mwenzi wako wa ndoa hebu kaeni chini myaweke mambo sawa ili 2021 iwakute mpo na furaha tele . Msijilimbikizie makosa kwenye ndoa yenu maana haitaleta afya katika ndoa ila migogoro ndio itazidi zaidi hatimaye ndoa itayumbayumba mnoo.

iv.  Kama wewe ni mwanafunzi, hebu jitathimini kwenye masomo yako je huwa unafanya vizuri au vibaya kwenye mitihani? Kama ni vibaya angalia sababu za kutokufaulu vizuri ni zipi halafu ujilekebishe mwaka 2021 uanze kwa kishindo kikubwa sanaaa. Labda huwa unachelewa kwenye vipindi au huudhurii darasani au hufanyi test,quiz au assignments n.k ..vyote hivyo ujirekebishe mpendwa yaani uwe mtu mpya mwaka 2021.

v.  Kama wewe ni mtumishi wa Mungu labda Mhubiri au mwimbaji n.k ,hebu jitathimini huu mwaka 2020 umefanya huduma kwelikweli ya kumtumikia Mungu kwenye nafasi yako?( Yeremia 48:10A imeandikwa;- Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu Jichunguze wewe uliyeokoka mahusiano yako na Mungu yakoje? Ili mwaka 2021 uweze kuwa karibu na Munggu zaidi.

vi.  Fanya tathimini kwenye Mahusiano yako wewe  na ndugu zako je yapoje? Pia na  Marafiki zako, wafanyakazi wenzako,Majirani zako,Wafanya biashara wenzako n.k..Kama kwenye familiya yenu kuna migogoro au kwenye ukoo wenu basi hakikisha wewe unayeusoma ujumbe huu ukawe chanzo cha kuhakikisha amani inapatikana, ili ugomvi uweze kuisha hatimaye mwaka 2021 muingie mkiwa wapya kabisa yaani mnafurahiana ndugu wote na wala kusiwe na matabaka yoyote.

 

5.      Weka malengo

Mpendwa hakikisha unaingia mwaka 2021 tayari ukiwa na malengo mapya kabisa ambayo ndiyo utakwenda kuyatekeleza.

Kuingia mwaka 2021 bila malengo inakuwa ni kama vile umeianza safari ambayo hujui unakokwenda ni wapi na utafika lini, mwisho wake mwaka unaisha hamna hata kitu cha maana ulichofanya, kwa sababu itakuwa unafanya hiki mara ufanye kile, mwisho wake unajikuta hakuna ulichokitimiza na mwaka unakuwa umeisha.

Kama upo kwenye ndoa, malengo mpange wote wawili sio mtu mmoja , na kila mtu ayafahamu malengo ili kama kuna mtu mmojawapo anataka kufuja pesa unamkumbusha mume wangu/mke wangu lakini kumbuka malengo tuliyoyaweka, kwa jinsi pesa zinavyotumika hivyo inaweza kupelekea tukashindwa kufikia malengo yetu. Lakini kama malengo yakiwekwa na mtu mmoja uwajibikaji nakuwa mdogo kwa mtu asiyeyafahamu wala hakushirikishwa kwenye kuyapanga malengo hayo.

Lakini kama kuna malengo ambayo hayajamalizika kutekelezeka mwaka huu 2020 basi ya bebe ukayatekeleze mwaka 2020.

Unapoweka malengo weka na mikakakati(strategies) ya kutekeleza malengo hayo, pia weka muda mwafaka(time frame) wa kila lengo kuhakikisha umelitimiza ndani ya muda huo. Mfano umeweka lengo la kuanza ujenzi 2021, kwahiyo labda unapanga kuanzia mwezi fulani nitafanya hivi, na kuanzia mwezi Fulani nitafanya hivi, vivyo hivyo mpaka mwaka unaisha kunakuta umetimiza kabisa.

 

6. Jitabirie mafanikio na mambo mazuri wala sio mabaya mwaka 2021.

Yakobo 3:10 imeandikwa;- Katika kinywa kilekile hutoka Baraka na laana, ndugu zangu haifai mambo hayo kuwa hivyo.

Mithali 18:21 imeandikwa;- Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi ,na wao waupendao watakula matunda yake.

Hivyo basi mpendwa kutokana na mistari hiyo utaona kwamba wewe uwezo wa kujitabiria mabaya au mazuri  upo ndani ya uwezo wako , maana kinywa kinaumba jambo, mfano kama wewe kila siku ni wa kusema mimi siwezi na kweli utakuwa huwezi maana unakuwa umejiumbia mwenyewe. Mungu alipokuwa unaumba dunia kwanza alitamka kwa kinywa chake na kweli ikawa katika uhalisia, mfano ukisoma kitabu cha Mwanzo 1:6 utaona uhalisia ninao uzungumza ambapo imeandikwa kwamba;- Mungu akasema na liwe anga katikati ya maji ,likayatenge maji na maji.

Mungu alivyotamka ndivyo ilivyokuwa , hivyo hivyo na kwako pia utakavyojitamkia kwa kinywa chako ndivyo utakavyokuwa. Mpendwa jitabirie mambo yaliyomema mwaka 2021 hakika utaona uhalisia wake.

Ubarikiwe sana mpendwa, nakutakia maandalizi mema ya kuupokea mwaka mpya 2021.

@Msufu- Desemba 31, 2020, www.msufu.blogspot.com, 0753255132

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

SOMO # 03: MAAJABU YA NAMBA SABA

SOMO # 01: ADUI

SOMO # 07: MAOMBI